JITAFAKARI KAMA UPENDO HAUNA NI BURE
Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.
1 KOR. 13:13 SUV
Wapenzi, siwaandikii amri mpya, ila amri ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Na hiyo amri ya zamani ni neno lile mlilolisikia. Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu; kwa kuwa giza linapita na ile nuru ya kweli imekwisha kung’aa. Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa. Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.
1 YOH. 2:7-11 SUV
Katika hayo matatu, imani, tumaini na upendo lililo kuu ni upendo. Tunahubiri kuhusu imani, Sawa. Tunalihubiri lile tumaini letu ndani ya Kristo, nayo ni sawa pia. Sema lililo kuu ni upendo.
Tufundishane upendo sana haya mengine yanajengeka katika hilo. Kwani amri mpya hakuna, kwani Yohana anasema anatuandika amri ile tulioisikia tangu mwanzo. Ile amri tuliyoisika mwanzo, ikajenga imani yetu kwa Yesu Kristo, nasi tukapata tumaini ndani yake ndiyo anayosema nasi. Tena ni amri mpya, akisema hivyo anaitofautisha na ile ya zamani, na amri mpya tuliyopewa si nyingine ni upendo. Anaendelea akizungumzia upendo wa ndugu; usipompenda ndugu yako haupo nuruni, hupo gizani haijalishi utasemaje. Na ukimpenda ndugu yako, wewe hupo nuruni tena unayo nuru, zaidi ya hapo wewe si kipofu hauendi gizani.
Kwa lugha ya mtume Paulo macho yako yanatiwa nuru, katika kuonyesha upendo wako kwa ndugu zako. Kama hauna upendo wewe ni kipofu, na unakwenda gizani, tafadhali usiutumie ule mstari mahalufu wa mtunga Zaburi, Eti neno lako ni taa miguuni mwangu, Eti linaniangazia njia zangu; si kweli. Kama hauna huu upendo kwa ndugu, basi hiyo taa haipo, wala huo mwangaza haupo. Fanya tu urudi nuruni tena. Njia ya kurudi ipo.
Yohana katumia sana neno ndugu, sema Yesu Kristo alisema jirani yako. Na sehemu nyingine akasema mpendane ninyi kwa ninyi kwa uo upendo ulimwengu utajua tumekuwa wanafunzi wake kweli. Hivyo napenda niitanue maana ya hili neno ndugu pasipo kwenda nje ya mukhtadha wake Kristo. Ndugu yako ni jirani yako, na jirani yako ni mtu yeyote yule anayaweza kuathirika na kutenda au kutokutenda kwako, hii ni kwa maneno au matendo. Yeyote yule atakayeathirika na maneno yako ni ndugu yako, hivyo chunga maneno yako yajae munyu ili kuwafaa hao.
Kwa matendo yako, tafadhali fanya vile ambavyo wewe ungependa watu wakufanyie.
Upendo ndio utimilifu wa sheria, kumpenda ndugu kuna unayemuona kuna fanya upendo wako kwa Mungu usiyemuona uwe ni wa kweli wala si unafiki. Maana ni unafiki ulioje kumpenda Mungu usiyemuona huku unamchukia ndugu yako, jirani yako unayemuona kila siku mtaani, unapanda nae daradara, unakula nae mgahawani, unafanya nae kazi ofisi moja. Si ajabu katika Mathayo 6:14 Mungu akaweka zuio kuwa kama haujamsamehe huyo ndugu jua kuwa na kwake msamaha hakuna.
Acha upendo utawale, tupendane kwa kweli. We amisha milima, tenda miujiza ya kila aina, kama upendo hakuna ni bure. Hivi unajua hata matoleo yako, pamoja na sadaka zako ni bure kama hazijafungwa kwenye kifurushi cha upendo.
Si ajabu Yesu Kristo alitutaka tuache sadaka madhabahuni bila ya kuitoa mpaka tukapatane na yule ndugu tuliyekosana nae.
Upendo ndio mkuu, acha utawale.
Na: Kelvin Kidifu
GBS ARUSHA