IJUE DHAMBI YA MAUTI
Nimesoma kitabu kimoja ninachokijua kuwa kimeandika kitu kuhusu dhambi ya mauti, ili nije kushirikiana nanyi. Nimemaliza hiyo sehemu, nimeambiwa niandike kile nimekipata. Hivyo basi acha nichukue niandike nilichopata, kwa lugha nyepesi kadri Roho Mtakatifu atakavyo niongoza.
Kama mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo, ninamaanisha, wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo. Jambo lo lote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti.
1 Yohana 5:16-17 NEN
Yohana kwenye waraka wake wa kwanza anaibua hili swala kwamba kuna dhambi mtu anaweza fanya zenye matokeo mawili tofauti. Zote ni dhambi sema moja ni ya mauti na nyingine si ya mauti. Na kama ndugu amefanya dhambi isiyo ya mauti, unaweza ukaomba Mungu akampa uzima. Hivyo ijulikane kuwa hiyo dhambi ya mauti inazungumzia mauti ya kiroho na sio ya kimwili. Kwani hakuna atendaye dhambi akiwa amekufa kimwili, bali ukifa kiroho kimwili bado unaishi. Hivyo basi hata kama ni mpendwa, tulikuwa tunasali pamoja kama umefanya dhambi ya mauti hakuna tena nafasi ya kupewa uzima na Mungu.
Dhambi ya mauti ni nini? Dhambi ya mauti ni ile hali muamini wa Yesu Kristo anapofanya dhambi inayopelekea mauti, mauti ya kiroho.
Hii inakuje, tusome neno hili;
Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu, na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo, wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.
EBR. 6:4-6 SUV
Hapo tunaona sio watu wote wanaweza kuifanya hii dhambi ya mauti, kwani hilo neno hapo juu linaweka vigezo vya mtu kutoweza kufanywa upya hata kama akitubu.
Kwa wazi kabisa watoto katika wokovu hili andiko haliwahusu. Kwani 1 Yohana 2:1 inasema watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,. Hivyo watoto yao ni maziwa yasiyoghoshiwa.
Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;
1 PET. 2:2 SUV
Vigezo hivyo vya mkristo anayaweza kufanya dhambi ya mauti ni:-
1. Awe amejitambua kuwa amepotea, na hawezi kujiokoa mwenyewe isipokuwa kumkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wake. (kuokoka) Yaani kuipokea nuru inayopatikana kweli ya Kristo.
2. Ni watu walioipokea zawadi au kipawa cha mbinguni. Yaani wale waliompokea Yesu Kristo kwani Yeye ndiye hiyo zawadi iliyotoka mbinguni. Yohana 3:16 Yesu alitolewa kama zawadi kwa ajili yetu.
3. Ni wale walioshiriki wa Roho Mtakatifu, hapa ni kujazwa Roho Mtakatifu na kushiriki karama zake pamoja na huduma zake.
4. Wale waliolionja neno zuri la Mungu. Hapa ni kuijua kweli, kulijua Neno la Mungu linasemaje na linamtaka mkristo afanye nini.
5. Ni wale walioonja nguvu za zamani zijazo, hapa ni pale umezitumia nguvu za Mungu katika Roho wake hii ni zaidi ya kunena kwa lugha na kukemea pepo.
Ukikizi vigezo hivyo basi Paul anasema ukianguka haiwezekani kufanywa upya hata kama wakitubu.
Kwani kwa kufanya hivyo wanamsulubisha Yesu Kristo mara ya pili katika nafsi zao. Tena kwa kufanya hivyo wanamfedhehi Yesu Kristo kwa dhahiri. Basi unaweza sema hii inakuwaje mtu mwenye vigezo hivyo akafanywa hivyo.
Soma neno hili hapa chini;
Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao. Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu. Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?
EBR. 10:26-29 SUV
Dhambi hiyo mtu akiifanya kwa makusudi basi hakuna tena dhabihu kwa ajili ya dhambi.
Sema kusudi hiyo ukisoma hapo chini katika ufafanuzi wake juu ya hilo Paulo anasema katika agano la kale mtu aliyeidharau sheria ya Musa alikufa bila huruma, hivyo basi inampasa adhabu kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema.
Fumbuka macho ndugu yangu. Kumkanyaga Mwana wa Mungu hapo ni kumkana Yesu Kristo.
Kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, ni kudharau wokovu na msamaha wa dhambi. Kudharau kazi ya msalaba.
Baya zaidi ni kumfanyia jeuri Roho wa neema. Hii inaonyesha kuwa huyu Roho wa neema alivyotaka kukulejesha mpaka hapo ulipomfanyia jeuri.
Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa.
MT. 12:31 SUV
Kila dhambi inamsamaha, taja zote unazoweza kuzisema ni dhambi. Sema ukiudharau wokovu huku umeonja hivyo vigezo basi hiyo ni dhambi ya mauti. Usimpe Yesu Kristo kisogo, usiache wokovu na kuanza kuhutukana. Usije sema Yesu sio Kristo. Usijesema huku ukiwa unajua eti Yesu hakuja katika mwili. Eti Yesu Kristo sio mkombozi wa ulimwengu. Ukiona umeteleza na kutenda dhambi Rudi haraka utubu, Tafadhali tubu.Kutubu kwako ni kielelezo kuwa hauidharau damu ya agano, wala kweli ya Mungu na Mwana wa Mungu. Kwani ukiomba utalitaja tu jina lake. Wengi wametenda dhambi na shetani akawadanganya kwamba dhambi zao hizo hazina msamaha tena, kumbuka Daudi alizini na mke wa mtu, kisha akaua, sema alipotubu alisamehewa. Kama Mungu anasamehe wazinzi na wauaji, wewe ni nani? Rudi ndugu yangu ili ni ombi langu kwako; rudi magotini hapo ulipo utubu Nawe utasamehewa. Chunga sana usijeanguka tena dhambini, sema ukianguka na Roho wa neema akakusihi urudi tafadhali rudi. Usiufanye moyo wako mgumu. Hii inadhihirishwa na huzuni ya ndani yako, ndani ya moyo wako kila unapofanya chochote kinyume na Neno la Mungu, kinyume na maelekezo ya Kristo Yesu, kinyume na kweli ya Kristo Yesu. Hiyo huzuni ni wito wako kuelekea toba; tubu sasa sio kesho kwani kuna zawadi ya uzima Mungu yu tayari kukupa tena Leo.
Na: KELVIN KIDIFU
GBS ARUSHA